2 Agosti 2017
Juzi, Mbowe akisoma maazimio ya kikao cha Kamati Kuu ya Chadema, alitoa tathmini ya hali ya uchumi ambayo pamoja na mambo mengine, alisema hali ya uchumi imekuwa tete katika awamu ya tano ya utawala ikilinganishwa na iliyopita.
Mbowe alitaja baadhi ya mambo ambayo yanaashiria kushuka kwa uchumi kuwa ni pamoja na hali ya ukata, kushuka kwa ununuzi wa bidhaa za ndani, kuongezeka kwa Deni la Taifa pamoja na kushuka kwa uwekezaji.
Lakini jana Serikali kupitia kwa msemaji wake, Dk Hassan Abbasi imesema uchumi uko imara na kuwataka wananchi waachane na ushabiki wa kisiasa.
Dk Abbasi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), aliwaambia waandishi wa habari kwamba uchumi wa dunia uliyumba mwaka uliopita na ndiyo maana hali ilionekana kuwa ngumu, lakini sasa imeimarika.
“Tanzania inapata heshima duniani. Jina Magufuli ni brand kwa sasa duniani kutokana na mambo anayoyafanya,” alisema. “Takwimu za BoT (Benki Kuu ya Tanzania) na Shirika la Fedha Duniani (IMF) pamoja na changamoto za duniani, lakini uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa imara na kiujumla unakua kwa asilimia 7.”
Akitumia takwimu mbalimbali za kitaifa na kimataifa, Dk Abbasi alitaja mambo mbalimbali ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imeyafanya ikiwamo kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato na kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi, rushwa na utoaji wa elimu bure.
Alisema tangu Serikali ya Rais Magufuli imeingia madarakani, kiwango cha mapato ya kodi kwa mwezi kimeongezeka kutoka Sh925 bilioni mwaka 2015 hadi Sh1 trilioni mwaka uliopita.
Kuhusu mfumuko wa bei, alisema umeshuka kutoka asilimia sita hadi asilimia tano wakati mwaka 2015 ulikuwa ni zaidi ya asilimia nane, “Wakati sisi tuko tano, Ukanda wa Afrika Mashariki ukomo wa mfumuko wa bei ni asilimia nane,” alisema.
Uwekezaji
Tathmini ya Chadema, ilieleza kutokuwapo mazingira bora ya uwekezaji nchini kutokana na masuala mbalimbali likiwamo la usafirishaji wa mchanga wa madini (makinikia).
Dk Abbasi alisema taarifa za kuwa uwekezaji umeshuka si za kweli na kwamba Tanzania ipo katika nafasi ya nane kwa Bara la Afrika na ya kwanza Afrika Mashariki kwa kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji, “Biashara nyingi zimefunguliwa kuliko zilizofungwa.”
Afya
Katika sekta ya afya, Dk Abbasi alisema katika miaka iliyopita, bajeti ya dawa 2015 ilikuwa Sh30 bilioni, lakini imeongezwa hadi Sh261 bilioni mwaka huu wa fedha ili kuhakikisha hospitali na vituo vya afya zinapata dawa na vifaa tiba.
Alisema ongezeko hilo litaboresha huduma za afya kwa Watanzania wengi.
Elimu
Msemaji huyo wa Serikali pia aligusia hoja ya elimu bure na kusema hilo limesimamiwa vyema na Serikali ya Rais Magufuli na kuhakikisha vifaa vya kusomea ikiwamo madawati vinapatikana kwa kila mwanafunzi.
“Jumla ya Sh18 bilioni zinatolewa kila mwezi kwa ajili ya kutekeleza mpango wa elimu bure,” alisema.
Alisema mikopo ya elimu ya juu imepewa kipaumbele ikiwamo kuongeza bajeti kutoka Sh341 bilioni hadi Sh475 bilioni mwaka huu. “Nchi yetu ina furaha na amani pamoja na changamoto zetu kama Taifa ni wajibu wa kila mtu achape kazi kwa maendeleo na siyo kushabikia siasa,” alisema.
Uhuru wa habari
Dk Abbasi ambaye kitaaluma ni mwanasheria na mwanahabari, alisema pia kwamba Taifa linatambua umuhimu wa vyombo vya habari na kutekeleza mikataba ya kimataifa.
“Tanzania ni moja ya nchi chache duniani zilizotunga Sheria ya Huduma ya Habari ambayo inampa uhuru mwanahabari,” alisema.
Alisema hadi sasa kuna magazeti 430, redio 140 na televisheni 32 nchini.
0 Post a Comment:
Post a Comment